ZURA YASIMAMIA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI KITUO CHA MAFUTA MELITANO, PEMBA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR. 

ZURA YASIMAMIA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI KITUO CHA MAFUTA MELITANO, PEMBA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR. 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA) imesimamia uwekaji wa Jiwe la Msingi Kituo cha Mafuta (Coastal Fuel Service) Melitano ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Jiwe hilo la Msingi limewekwa Leo Tarehe 29/12/2023 katika eneo la Melitano, Pemba ambapo Mgeni rasmi alikua Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid.

Kituo cha Mafuta (Coastal Fuel Service) kilianza mpango wa ujenzi wa Kituo cha Mafuta mnamo tarehe 11 Novemba, 2020 baada ya kuwasilisha ombi ZURA na kuanza ukaguzi wa eneo kwa kuzingatia

haja kisheria baada ya kutoa mita 15 kutoka katikati ya Barabara kongwe inayotoka Chake Chake kuelekea Wete na Barabara mpya inayotokea Melitano kuelekea Konde.

ZURA imehakikisha ujenzi wa kituo hiki unazingatia usalama wa wananchi wanaotumia Barabara kwa kuacha mita 50 kutoka katika makutano ya Barabara, na mita 50 kutoka mpindo uliopo katika Barabara inayoelekea Konde kama ilivyoainishwa katika kifungu nambari 20(2) cha Kanuni ya Usimamizi wa Vituo vya Mafuta ya 2019, ambayo imefanyiwa marejeo mwaka 2022.

 

Katika kuhakikisha kituo hiki kinafikia malengo ya kuanzishwa kwake na kuwanufaisha wanajamii wa eneo hili, tarehe 30/08/2021 Mamlaka ilifanya mkutano ya wazi (Public Hearing) kwa mujibu wa kifungu nambari 36 cha Sheria ya ZURA namba 7 ya 2013.

Mkutano huo ulishirikisha wananchi wa Shehia hii ya Mbuzini, Taasisi wadau ikiwemo, Kamisheni ya Ardhi, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA), Idara ya Nishati na Madini Zanzibar, Wakala wa Barabara,  Idara ya Mazingira, na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake.

Kwa kuwa haikutokezea mdau aliyetoa pingamizi yoyote juu ya mradi huu ZURA ilitoa kibali kwa mwekezaji wa Kituo hiki cha Mafuta Melitano ili kuanza Ujenzi wa kituo hiki Tarahe 15/11/2021.

Aidha, ZURA imeendelea kufanya ukaguzi wa ujenzi wa kituo hiki kuanzia hatua ya awali kwa kutoa miongozo na maelekezo ya Kikanuni ikiwemo kujenga Paa la kituo lenye urefu usiopungua mita 5 na upana usiopungua mita 12, kutenganisha pampu moja ya mafuta na pampu nyengine kwa umbali usiopungua mita 7, kutenganisha eneo la kuuzia mafuta na majengo mengine kwa masafa yasiyopungua mita 8, pamoja na kuhakikisha uwepo wa vyoo viwili kwa ajili ya wanawake na wanaume.

 ZURA itaendelea kusimamia na kutoa miongozo ya kukamilisha ujenzi huu kwa kuzingatia ujengaji wa sakafu ya zege unakua madhubuti katika eneo lote la mbele na eneo la matangi ya kuhifadhia mafuta, kuweka bango la bei lenye kutoa mwanga (illuminating price board), kujenga mitaro na hodhi la chini la kutenganisha mafuta na maji (oil-water separater) ambalo litasaidia kuzuia ueneaji wa mafuta aridhini kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

Kituo cha Mafuta (Coastal Fuel Service) kilichopo Melitano, Pemba kinatarajia kukamilisha Ujenzi wake Mwezi Machi, 2024 na kuongeza idadi ya vituo vya mafuta vinavyotoa huduma Pemba kufikia 20, jambo ambalo litaimarisha upatikanaji wa huduma ya Mafuta hasa kwavile kitatoa Huduma kwa masaa 24.