BOHARI YA KWANZA YA GESI YAFUNGULIWA ZANZIBAR

BOHARI YA KWANZA YA GESI YAFUNGULIWA ZANZIBAR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi Leo Tarehe 27/06/2024 amefungua rasmi Bohari ya kwanza ya kuhifadhia Gesi ya Kampuni ya Oryx Gas Zanzibar Limited iliyopo Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wakati akifungua Bohari hiyo Rais Dkt. Mwinyi alitoa maelekezo kwa ZURA kutafuta namna ya kuwezesha kupatikana gesi kwa bei nafuu, ili wananchi wamudu bei ya bidhaa hiyo.

Rais Dkt.Mwinyi pia alitoa rai kwa wananchi kuondokana na matumizi ya makaa na kuni hatua na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi, ili kupunguza athari za mazingira pamoja na kujiepusha na athari za kiafya zinazotokana na hewa sumu.

Bohari iliyofunguliwa ni ya Kampuni ya ORYX Gas Zanzibar Limited ambayo ina matangi yenye ujazo wa tani 1,388 ambazo ni sawa na takriban kilo 1,388,000 za gesi.

Bohari hii inakwenda kuchukua asilimia kubwa ya mahitaji ya gesi ya Zanzibar ambapo kwa Mwaka 2023 gesi iliyotumika Zanzibar ni kilo 9,340,670 ikiwa ni ongezeko la asilimia 177 kutoka kilo 5,276,847 kwa Mwaka 2019.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZURA ambayo ipo chini ya Wizara ya Maji, Nishati na Madini imekua ikihamasisha matumizi ya gesi kwa Wanchi na kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama gesi kupitia Kampeni maalum, Mikutano ya Umma, Vipindi vya Redio na TV pamoja na Mitandao ya Kijamii.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mpango Mkuu wa Miaka 10 wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia, ambapo kufikia 2034 zaidi ya asilia 80 ya Watanzania wanatakiwa wawe wamehamasishwa na wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi.