TAARIFA KUHUSU HALI YA MAFUTA YA TAA ZANZIBAR

TAARIFA KUHUSU HALI YA MAFUTA YA TAA ZANZIBAR

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) inapenda kuwajulisha Wananchi ya kwamba kuna changamoto ya upungufu wa Mafuta ya Taa kwa baadhi ya vituo tangu mwishoni mwa Mwezi Julai 2020.

Hali hiyo ilitokana na Mafuta ya Taa kutonunuliwa kwa muda wa Miezi mitatu kutoka nje ya nchi kwasababu Mafuta ya Taa huagizwa sambamba na Mafuta ya Ndege, pia kutokana na mripuko wa Maradhi ya Corona (Covid-19) Mafuta ya Ndege hayakuagizwa kwa vile kuna akiba ya kutosha ya Mafuta ya Ndege.

Kutokana na hali hiyo ZURA ilifanya jitihada ya kuzungumza na Kampuni ya PUMA ili kuzipatia Kampuni nyengine Mafuta ya Taa. Baada ya hapo Mafuta ya Taa yalipatikana tena Zanzibar mpaka pale ilipotokea changamoto ya Ajali ya moto katika Kampuni ya PUMA mnamo tarehe 21 Julai, 2020, na kupelekea kuungua kwa miundombinu yote ya upakizi wa mafuta ya kampuni hiyo.

Kutokana na kutokea kwa ajali hiyo, ZURA kwa kushirikiana na Kampuni ya United Petroleum (UP) imechukua hatua ya kwenda kuchukua mafuta ya taa kutoka nchi jirani ya Kenya (Mombasa) kwa ajili ya kuondoa changamoto ya upungufu wa Mafuta ya Taa Zanzibar.

Meli ya United Spirit tayari imeshawasili katika Bandari ya Mombasa na ipo tayari kwa ajili ya upakizi wa Mafuta ya Taa baada ya ushushaji wa mafuta ya Kampuni za Kenya unaoendelea. Meli hiyo inatarajiwa kupakia Lita Laki Sita (600,000) za Mafuta ya Taa Tarehe 10 Agosti, 2020 na kufika Zanzibar Tarehe 12 Agosti, 2020.

Sambamba na hilo kampuni ya United Petroleum (UP) itatoa kiwango cha mafuta kilichobakia ambacho ni Lita 26,388 kwa ajili ya kusambazwa Vituoni mpaka hapo Meli yake ya Mafuta itakapowasili na na Mafuta ya Taa.

ZURA inawaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kueleza kwamba inafuatilia kwa karibu changamoto hii ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa Mafuta ya Taa nchini inarejea kama kawaida.

Aidha, Mamlaka inawaonya Wamiliki wa Vituo vya Mafuta kutouza Mafuta kwa Bei ambazo si rasmi na hatua kali zitachukuliwa kwa atakaekwenda kinyume.